Mchango wa Sekta ya Madini nchini umeendelea kukua hadi kufikia asilimia 9, ikiwa ni katika kipindi cha miaka miwili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan madarakani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachimbaji wadogo wa dhahabu Wilayani Nzega mkoani Tabora wamesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa Serikali kupitia Tume ya Madini, hali iliyopelekea kuongezeka kwa uzalishaji kutokana na wa matimizi ya teknolojia za kisasa.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa eneo hilo, Peter Mashiri wa Kikundi cha Msilale cha Nzega amesema kuongezeka kwa mapato hayo pia kumetokana na jitihada za Serikali za kuhakikisha makundi yote yanashiriki kwenye sekta hiyo.
Amesema, “vijana wanaozunguka mgodi hadi sasa ni zaidi ya 48 ambao wameajiriwa, tunaipongeza Serikali kwa kuwajali wachimbaji wadogo na kutoa leseni kwa makundi hayo tunaiomba iendelee kuwagawia maeneo ambayo bado yanamilikiwa na wachimbaji wakubwa bila kuendelezwa.
Kwa upande wake Katibu wa kikundi hicho, Magreth Emmanuel amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Sekta ya Madini kwa kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi na kwamba uwepo wa Sekta ya Madini umefungua fursa na hamasa kwa wanawake ambao kwasasa wameanza kujihusisha na shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, na biashara ya madini.
Naye Msimamizi wa Mazingira wa kikundi hicho amesitiza kuwa mgodi huo umeendelea kuboresha mazingira yake kwa kuweka mitambo ya kisasa ambayo inawasaidia kuingia na kutoka ndani ya migodi, tofauti na awali ambapo walikuwa wanatumia kamba kushuka chini jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa usalama wao.