Vinara wa Ligi Kuu ya England klabu ya Arsenal huenda ikamkosa Beki wake kutoka nchini Ufaransa William Saliba kwenye mchezo ujao wa Ligi hiyo utakaowakutanisha na Majogoo wa Jiji Liverpool.
Miamba hiyo itakutana keshokutwa Jumapili (April 09) kwenye Uwanja wa Anfield, huku Arsenal ikihitaji ushindi zaidi, ili kuendelea kuwa katika mbio za kuwania Ubingwa wa England msimu huu 2022/23.
Beki Saliba amekuwa nguzo muhimu ya ulinzi katika kikosi cha Arsenal ambapo msimu huu ametengeneza kombinesheni kali na Beki kutoka nchini Brazil Gabriel Magalhaes.
Saliba alikosekana katika Michezo miwili iliyopita ambayo Arsenal imeshinda, baada ya kuumia kwenye mchezo wa Europa League dhidi ya Sporting CP ya Ureno.
Ripoti zinaeleza kuwa, Saliba bado anapambana kuwa sawa huku majeraha yake ikielezwa kuwa huenda yakamuweka nje kwa muda mrefu zaidi.
Kukosekana kwake katika michezo miwili iliyopita kumeweza kumpa nafasi Rob Holding kuziba nafasi yake.
Meneja wa kikosi cha Arsenal, Mikel Arteta amenukuliwa akisema: “Matumaini yangu ni kuona Saliba anapona kabla ya msimu kumalizika, kuumia mgongo sio kitu kidogo ndiyo maana madaktari wanaendelea kupambana kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.
Arsenal inakwenda kukutana Liverpool ikiwa inamiliki alama 72 kileleni, ikifuatiwa na Mabingwa watetezi Manchester City yenye alama 64 huku Majogoo wa Jiji wakiwa katika nafasi ya nane kwa kumiliki alama 43.