Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Akson ameitaka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kukaa pamoja na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora ili kuja na mfumo utaowatambua Watumishi wanaojitolea katika maeneo ya kutolea huduma, ili wapewe kipaumbele pindi nafasi za ajira zitakapotolewa.

Dkt. Tulia ameyasema hayo Jijini Dodoma katika Mkutano wa 11 kikao cha tatu, wakati Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akitoa majibu kwa Mbunge wa viti maalum, Felister Deogratius Njau juu ya ajira kwa Watumishi wanaojitolea katika vituo vya kutolea huduma. 

Amesema, “Waziri wa afya na Waziri wa TAMISEMI nafikiri kuna haja ya kukaa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Watumishi wa afya wanaojitolea na walimu wanaojitolea huwa haipendezi sana, wao ndio hawana sifa za ajira au, nafikiri utengenezwe utaratibu mzuri ili kila mwaka kuwe na taarifa za wanaojitolea ajira zinapopatikana wapewe kipaumbele.”

Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Akson.

Awali, Dkt. Godwin Mollel alisema Wizara ya Afya imetoa mwongozo wa kuwalipa nusu mshahara kwa mapato ya ndani Watumishi wanaojitolea, huku akisisitiza hospitali za Mikoa, Kanda na Taifa zimeweza kuwalipa hadi 40% ya Watumishi wote wanaojitolea mshahara kamili kwa mapato ya ndani. 

Amesema, Wizara itashirikiana na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora ili kuona namna bora ya kuwapa kipaumbele Watumishi ambao wamekuwa wakijitolea kwenye vituo vya kutolea huduma kuliko waliopo nje wakisubiri ajira ambapo ameongeza kuwa Wizara itaendelea kupeleka Watumishi katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma bora. 

Saba washikiliwa na Polisi kwa mauaji, ufukuaji makaburi
Kocha Hans amkataa Mkude Singida Big Stars