Kiungo kutoka Visiwani Zanzibar na klabu ya Young Africans Mudathir Yahya Abbas amefichua siri ya bao lake alilofunga dhidi ya TP Mazembe ambalo limeibuka Bao Bora la Kombe la Shirikisho Afrika Hatua ya Makundi kwa kusema Kocha Nasreddine Nabi alihusika.

Mudathir amesema, siri ya bao hilo ilitokana na maelekezo ya Kocha Nabi ambapo alimwambia siku hiyo kuwa ahakikishe anacheza nyuma ya washambuliaji wake ili yakitokea makosa afunge.

“Namshukuru Mungu kwa bao hilo ambalo naweza kusema nilifunga kwa msaada mkubwa wa makocha ambapo waliniambia siku hiyo nihakikishe nacheza nyuma ya washambuliaji jambo ambalo nilifanya hivyo na kujikuta nafanikiwa kupata nafasi ya kufunga,” amesema Mudathir.

Kiungo huyo aliifungia Young Africans bao la pili baada ya Mshambuliaji Kennedy Musonda kutangulia kuifungia klabu hiyo katika ushindi wa mabao matatu dhidi ya TP Mazembe jijini Dar es salaam.

Bao lingine ya Young Africans siku hiyo lilikwamishwa wavuni na Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Tuisila Kisinda.

Bao la Mudathir Yahya dhidi ya TP Mazembe limepigiwa kura na mashabiki kupitia ukurasa wa Twitter wa CAF na kupata asilimia 70.5, akifuatiwa na Aymen Mahious wa USMA akifunga bao dhidi ya FC Lupopo (20.8%), Aubin Kramo Kouamé wa ASEC Mimosas akipata  5.2% ya kura akiafunga dhidi ya Diables Noirs na Bao la Paul Acquah wa Rivers United alilofunga dhidi ya DC Motemba Pembe kwa kupata 3.5%.

Jumla ya kura zilizopigwa katika mchakato huo wa Bao Bora la Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika ni 84,166.

Twaha Kiduku: Ninabadili mfumo wa kuwachapa
Maandalizi uchaguzi Serikali za mitaa, 2025 kuendelea