Aprili 23 ngumi zitapigwa sana tu jijini Dodoma, wakati bondia maarufu nchini, Hassan Mwakinyo atakapopanda ulingoni dhidi ya Kuvesa Katembo wa Afrika Kusini, lakini pambano hilo likisaidia kuwanufaisha mabinti waliolamba dili ya Sh35 milioni.
Lengo la pambano hilo ni kusaidia kupata pesa za kununua taulo za watoto wa kike na inatakiwa idadi ya 40,000 zitakazogawiwa kwa wanafunzi wa mikoa wa nyanda za juu Kusini na kabla ya mabondia hao kupanda ulingoni, tayari kampuni ya Softcare Sanitary Pads imetoa taulo 20,000 na fedha na kwa pamoja vina thamani ya Sh35 milioni, ili kuunga mkono juhudi hizo kwa wanafunzi wa vijijini.
Promota wa shindano hilo, Sophia Mwakagenda, ambaye pia Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, amesema katika kuona umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike waliamua kuandaa pambano hilo ili kuchangia taulo za kike ili ziwasaidia kuondoa vikwazo kwenye masomo yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Dorrycare Technology Company, Victor Zang amesema lengo la pambano hilo ni kuchangisha fedha za kununua angalau taulo za kike 40,000 na kuzipeleka kwenye jamii.