Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Melis Medo ameomba umoja na mshikamano kwa viongozi na wadau mbalimbali wa michezo ili kuinusuru timu hiyo isishuke Daraja msimu huu.

Dodoma Jiji ni miongoni mwa timu sita zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja kutokana na nafasi iliyopo kwenye msimamo na idadi ya alama iliyokusanya katika michezo 25 iliyocheza mpaka sasa.

Kocha huyo ameeleza kuwa nafasi ya 11 waliyopo siyo salama sana kwao hivyo wanahitaji kushinda michezo mitano zilizobaki ili kuondoka hapo walipo na kupanda kwenye nafasi za katikati ya msimamo.

“Mimi na wenzangu wa benchi la ufundi tunafanya kazi yetu sawa na wachezaji kazi iliyobaki ni viongozi wetu kuweka umoja na mshikamano kati wadau wa michezo na wakazi wa Dodoma ili kuisapo-ti timu yao ikiwepo kuja kwa wingi uwanjani ili kuwapa hamasa wachezaji hasa katika mechi za nyumbani,” amesema Medo.

Kocha huyo amesema anahitaji kushinda michezo minne kati ya mechi tano zilizobaki ili kujiweka sehemu salama na anaamini kwa juhudi ambazo wanazifanya ya kuiandaa timu yao ukiunganisha na umoja na mshikamano kutoka kwa wakazi wa mkoa huo timu hiyo haitoshuka Daraja.

Amesema anatambua ushindani kwa sasa ni mkubwa lakini kama kutakuwa na kampeni ya mkoa katika mechi zilizobaki hakuna kitakacho washinda na Dodoma Jiji itamaliza msimu ikiwa bora.

Dodoma Jiji kesho Jumapili (April 09) inatarajiwa kuikabili Coastal Union ya Tanga, kwenye mchezo ambao utapigwa uwanja wa Jamhuri Dodoma na kocha huyo amesema lazima wachukue pointi tatu ili kuweka hai matumaini yao.

Ujenzi barabara kurahisisha usafirishaji, utoaji wa huduma
Sakata la maandamano Kenya: Odinga akubali kiaina matakwa ya Ruto