Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imedhamiria kuvifanyiwa marekebisho viwanja saba vya soka, baada ya tathmini kukamilika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Said Othman Yakub, Viwanja hivyo ni vile ambavyo vilitengewa Shilingi Bilioni 10 bilioni katika bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2022/2023.

Viwanja vitano kati ya hivyo, vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na vingine ni kile cha Uhuru na Mkapa vyote vipo jijini Dar es salaam.

Katibu Said Othman Yakub amesema baada ya kuidhinishiwa fedha hizo, walimpata mkandarasi mshauri ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), aliyezunguka katika viwanja vyote vinavyotarajiwa kufanyiwa maboresho kuangalia kinachopaswa kufanyika.

“Kwa hatua ya kwanza ya ukarabati vitaanza viwanja saba vilivyopo katika majiji, ambavyo ni Jamhuri (Dodoma), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Sokoine (Mbeya), CCM Kirumba (Mwanza) na Mkwakwani (Tanga), lakini ukarabati huo utavihusisha viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa.”

“Kuna maboresho makubwa yatafanyika katika viwanja hivi, baadhi vitaongezewa majukwaa, vingine vitaboreshewa vyumba vya kubadili nguo wachezaji na vingine vitaboreshewa nyasi za uwanja (pitch),” amesema Yakub.

Amesema Uwanja kama wa Benjamini Mkapa utajengwa na wakandarasi wawili huku mmoja akiwa wa kimataifa ili kuupa hadhi kubwa.

“Uwanja wetu kwa sasa unaweza kutumika katika michuano ambayo Simba na Yanga zinashiriki, lakini Super League ambayo Simba imechaguliwa kushiriki hauwezi kutumika kwa sababu ina viwango vikubwa hivyo tunataka kuufanyia maboresho zaidi.” amesema

Raizin ataja sababu za kushangilia dhidi ya Coastal
Bunge laidhinisha sheria adhabu kali ukatili dhidi ya Wanawake