Kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya kilimo katika eneo la utafiti kutoka Shilingi bilioni 11.5 hadi Shilingi bilioni 40.7 kwa mwaka wa fedha 2022/23, TARI-Dakawa kwa msimu huu wa kilimo, inatarajia kuzalisha tani 150 za mbegu za zao la mpunga kutoka tani 104 zilizozalishwa msimu uliopita.

Meneja TARI – Kituo cha Dakawa, Dkt. Jerome Mghase ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO jinsi ongezeko la bajeti ya utafiti lilivyowasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu za zao hilo.

Amesema, katika bajeti hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita imeiwezesha TARI-Dakawa fedha takriban Shilingi milioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kuhifadhia mbegu ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 300 za mpunga.

“tumepata fedha zingine jumla ya Shilingi milioni 90 kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambazo zimeongeza maeneo ya uzalishaji wa mbegu kutoka ekari 80 hadi ekari 120 ambazo zimeendelea kuongeza wigo wa uzalishaji mbegu wa zao hili”. Alisema Dkt. Mghase.

Dkt. Mghase ameongeza kuwa, kutokana na mahitaji ya mbegu bora nchini kuongezeka mwaka hadi mwaka, taasisi hiyo imejipanga kupanua eneo la uzalishaji wa mbegu za zao hilo katika maeneo mengine hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya mahitaji hayo.

Akizungumza kuhusu mbegu bora zinavyowafikia wakulima, Mratibu Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano kutoka TARI-Dakawa, Fabiola Langa amesema ili kuhakikisha teknolojia bora za kilimo zinawafikia wakulima wanaweka mashamba mfano hasa kwenye maeneo ya wakulima.

Kwa upande wake Mkulima wa zao hilo, Nasibu Katoto amesema kuwa kilimo chake kimeboreshwa kutokana na maelekezo, mafunzo na mbegu bora kutoka katika taasisi hiyo, na kuwashukuru wataalam wa taasisi hiyo kwa kuwashirikisha wakulima kuelezea changamoto ya mbegu wanazozitumia ili waendelee na utafiti na kuleta mbegu bora.

Jafo awataka Wachimbaji kufuata Sheria ya Mazingira
Chalamila aikubali Timu makabiliano ugonjwa wa Marburg