Uongozi wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad Casablanca kutoka Morocco, umepanga kuutumia mchezo wa Kariakoo Dabi kusoma zaidi mbinu za Simba SC kabla ya kukutana kwenye mchezo wa Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC itakuwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kati ya April 21 kuikaribisha Wydad Casablanca katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali kabla ya kwenda mjini Casablanca kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa kati ya April 28.
Taarifa kutoka jijini Dar es salaam zinaeleza kuwa tayari makachero wa Wydad Casablanca wameshawasili jijini humo kwa ajili ya kuwafuatilia kwa ukaribu Simba SC ambao Aprili 16 mwaka huu, watapambana na Young Africans katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hata hivyo Uongozi wa Simba SC unadaiwa kupata taarifa zote za ujio wa Makachero hao ambao wanadaiwa kufika jijini Dar es salaam tangu Ijumaa wakiwafuatilia kila hatua wanayoipiga.
Mtoa taarifa hizi amesema makachero hao wa Wydad Casablanca tayari wamewaona Simba katika mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports waliocheza dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar ambao Simba ilishinda 5-1.
Ameongeza kuwa, makachero hao wamepanga kuungalia mchezo wa Kariakoo Dabi utakaozikutanisha Simba SC dhidi ya Young Africans utakaopigwa Aprili 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
“Baadhi ya viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wydad Casablanca wapo hapa nchini tangu wiki iliyopita wakiifutilia Simba.ā
“Mara baada ya mchezo wa Kariakoo Dabi utakaowakutanisha Simba dhidi ya Young Africans, wataondoka wakiwa na mafaili yote ambayo watakayakabidhi kwa Benchi lao la Ufundi.
“Kama uongozi tulifahamu hilo, hivyo hatuna hofu kwani na sisi tumepanga kuwawahisha viongozi wetu huko Morocco kwa ajili ya kuwafuatilia wapinzani wetu hao.ā
“Hiyo haitufanyi tuwaogope na badala yake tunaendelea na maandalizi yetu kwa ajili ya mchezo huo,” amesema mtoa taarifa hizi
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa: “Tunafahamu kila kitu kinachoendelea, kama uongozi kila mchezo uliopo mbele yetu tunauchukulia kama fainali.”