Meneja wa Man United, Erik Ten Hag anadaiwa kuwinda saini za wachezaji wawili wa Brighton, Moises Caicedo na Alexis Mac Allister ili kuimarisha safu ya kiungo ya kikosi chake ili kuwapunguzia mzigo Bruno Fernandes, Casemiro na Christian Eriksen msimu ujao.
Inaripotiwa kuwa ili kuwapa nyota hao United itawagharimu zaidi ya Pauni Milioni 70.
Caicedo na Mac Allister wote wamekuwa viungo bora wa Brighton msimu huu na hivyo kuendeleza harakati za klabu hiyo kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Licha ya kwamba wote wawili wamesaini mikataba mipya hivi karibuni, huku Mac Allister akiwa amesaini kabla ya Kombe la Dunia mwaka jana na Caicedo aliweka hadharani nia yake ya kuondoka inategemewa na klabu gani itahitaji saini yake.
Mtandao mmoja wa majuu umeripoti kuwa wachezaji wote wawili wako kwenye orodha fupi ya wachezaji wanaoweza kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya joto ingawa Brighton hawana haja ya kuuza wachezaji kwa sasa.
Caicedo, 21, alitaka kujiunga na Arsenal Januari mwaka huu lakini alikaziwa na klabu yake.
“Nadhani aliteseka katika dirisha la usajili, wakati huo ulikuwa mgumu sana kwake,”
meneja wake, Roberto De Zerbi, alisema mwezi uliopita na kuongeza: “Lakini tunaweza kuelewa kwa sababu yeye ni mdogo sana. Anaweza kuteseka katika hali hii. Ingawa sasa anaweza kuwa sawa kucheza timu nyingine.”
Mkataba mpya wa Caicedo unamalizika mwaka 2027 huku wa Mac Allister, 24, ukitarajia kumalizika 2025.