Beki kutoka nchini Senegal na klabu ya Chelsea Kalidou Koulibaly amesema Meneja wa muda wa klabu hiyo Frank Lampard, anaweza kuiongoza timu hiyo kutoka katika kipindi kigumu inachopitia sasa.

Lampard, mwenye umri wa miaka 44, aliteuliwa kuwa Meneja wa muda wa Chelsea juma lililopita, akichukua nafasi ya Graham Potter, aliyetimuliwa kutokana na mwenendo mbovu.

Chelsea ipo katika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na alama 39 katika michezo 30 iliyocheza.

Pia, timu hiyo leo Jumatano (April 12) itavaana na Real Madrid katika mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, utakaochezwa Uwanja wa Santiago Bernabeu, nchini Hispania.

Akimzungumzia kocha huyo mpya Koulibaly amesema, Lampard mkongwe ni anayeijua vyema Chelsea hivyo anaamini anaweza kuiongoza timu kufanya vizuri msimu huu.

“Tunajua amewahi kucheza hapa, nawafahamu nusu ya wachezaji wa hii timu. Katika mazoezi amekuwa akitupa hamasa kutuahidi kutusapoti hadi mwisho na atatusaidia kutoka katika hali hii (kufanya vizuri),” amesema.

“Tunajua ni hali ngumu kwa kila mmoja, ikiwemo klabu, kocha na mashabiki, lakini tutatoa kila kitu ili kutoka katika hali hii na kuwafanya kuwa na furaha,” ameongeza beki huyo mwenye umri wa miaka 31.

Koulibaly raia wa Senegal, amesema lengo la kwanza la timu hiyo ni kushinda michezo yao na kuwafanya mashabiki kuwa na furaha.

Serikali yatangaza ajira mpya 21,200 kwa Walimu, Afya
Miaka 39 kumbukizi ya EDWARD MORINGE SOKOINE