Tarehe kama ya leo (April 12), miaka 39 iliyopita taifa lilipoteza kiongozi shupavu, Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine, ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilitangazia Taifa kuwa kijana wetu alipokuwa anatoka Dodoma amepata ajali eneo la Dakawa Morogoro na amefariki dunia.

Hakika Taifa lilipoteza kiongozi shupavu, aliyepinga ufisadi kwa vitendo kwa mkono wa chuma mafisadi wahujumu uchumi walimuogopa kama ukoma, mwaka 1982/83 aliendesha operation iliyoitwa uhujumu uchumi wote waliohusika waliipata kisawasawa, nchi mzima.

Watu walikuwa wanakwenda kutupa vitu vya thamani walivyokwapua baharini, na katika moja ya hotuba yake ya mwisho alipofunga kikao cha Bunge pale Dodoma, alisema wale wote wanaohusika tutakutana Dar es salaam kikao kinachofuata, lakini hakufika Dar es salaam.

Aliwahi kuwa Waziri Mkuu mara mbili, kuanzia Februari 13, 1977 hadi 7 Novemba 1980, halafu tena tangu Februari 24, 1983 hadi kifo chake, mara baada ya kupata ajali ya gari na kifo chake kilileta majonzi kwa Watanzania ambao alikuwa akiwatetea wanyonge na kuinua hali ya maisha yao.

Edward Moringe Sokoine alizaliwa Agosti 1,1938 na alifariki Aprili 12, 1984 na katika kumpa heshima yake, Chuo cha Kilimo na Mifugo Morogoro kilipewa jina la “Chuo cha Kilimo cha Sokoine” ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Sokoine.

Kalidou Koulibaly: Lampard anatosha Chelsea
Kagera yapokea Bilioni 2 ujenzi Kituo magonjwa ya mlipuko