Jeshi la Polisi Mkoani Njombe, linamshikilia mtu mmoja ambaye ni mfanyabiashara akikabiliwa na tuhumiwa za kuchoma moto duka lake na mengine ya jirani zake akilenga kujipatia faida kutokana na bima aliyokata ya biashara.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah amesema mtu (jina linahifadhiwa), alitekeleza tukio hilo April Mosi 2023 kwa kuchoma moto milango ya maduka, mali ya Jumuiya ya Wanawake wa CCM – UWT Wilaya ya Njombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah

Amesema, “Vibanda takribani 7 na mali zake ziliteketea mtuhumiwa tumemkamata na atafikishwa Mahakamani kwasababu alifanya hivyo kwa tamaa zake akijua hawezi kugundulika na alikuwa na lengo ajipatie faida lakini sasa hivi faida imekuwa hasara.”

Aprili Mosi, 2023, ilitokea taarifa ya moto majira ya 3:28 jumla ya maduka 21 kati ya 110 yanayomilikiwa na wafanyabiashara mbalimbali kwenye jengo la Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM, UWT Wilaya ya Njombe, kuwa yaliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya vitu na mali.

Sehemu ya Fremu za Maduka zilizoteketea kwa moto Aprili Mosi 2023, Njombe.

Akizungumza mara baada ya tukio hilo, Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Emmanuel George alisema chanzo cha awali cha moto huo kiligundulika kuwa ni hitilafu ya umeme na kwamba uchunguzi wa kina ulikuwa ukiendelea na kudai taarifa kamili itatolewa baadaye.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Njombe, Julius Peter alilipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Wananchi kwa kujitokeza kuzima moto huo pamoja na kuokoa mali na vitu mbalimbali vya Wafanyabiashara.

Kocha Singida Big Stars amtaja Fiston Mayele
Kevin de Bruyne azua hofu Manchester City