Aliyekuwa Kocha Mkuu wa KMC FC, Hitimana Thierry amesema hana kinyongo na Uongozi wa klabu hiyo na kilichotokea ni sehemu ya mchezo wa Soka, hivyo maisha lazima yaendelee.

Hitimana juzi Alhamis (April 13) alifikia makubaliano ya kuuvunja mkataba wake na mabosi wa KMC FC baada ya pande hizo mbili kukubalina kutokana na mwendo mbovu wa timu hiyo.

Mchezo wake wa mwisho kukiongoza kikosi hicho walifungwa mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold. Kwenye msimamo KMC ipo nafasi ya 14 ikiwa na alama 16.

Hitimana amesema kuwa hakuna tatizo lolote ambalo linaweza kumfanya auchukie Uongozi wa KMC FC, badala yake anaamini kilichotokea ni sehemu ya maisha ya Soka.

Amesema kwa muda wote aliokuwepo klabuni hapo aliishi vizuri na kila mmja, lakini alitambua kuna siku angeondoka na kuanza maisha mapya nje ya KMC FC.

“Kwa yaliyotokea hakuna tatizo lolote na hakuna shida ndiyo mpira wetu, nilikuwa KMC FC kwa ajili ya kufanyakazi na nilikuwa na uhusiano mzuri na kila mtu”

“Katika maisha unatakiwa kufahamu ipo siku utaondoka pale ulipokuwepo, na ndivyo ilivyokuwa kwangu, kwa hivyo niliamini kuna siku ningekuwa na maisha nje ya KMC FC.” amesema Hitimana.

Kwa sasa KMC ipo chini ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye alitambulishwa kuchukua mikoba ya Hitimana.

TIC yahudumia miradi 1,038 ya wawekezaji
Pugu Sekondari kuja na mkakati uendelezaji utoaji wa Viongozi