Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, Julian Nagelsmann amekaribishwa Chelsea awasilishe malengo yake kuhusu klabu hiyo kama sehemu ya mchakato wa chama hilo la Stanford Bridge kusaka kocha.

Hivi karibuni kocha huyo alitimuliwa kazi na FC Bayern Munich na nafasi yake ikachukuliwa na Thomas Tuchel ambaye naye alianza kwa kipigo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutokana na uwepo wake sokoni, Nagelsmann anahusishwa na timu kibao za Ulaya ikiwemo Chelsea ambayo inatafuta kocha mpya atakayerithi mikoba ya Graham Potter.

The Blues ilimtimua Potter mwezi huu kabla ya kumteua Frank Lampard kama kocha wa muda, huku ikiendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya.

Mmiliki wa klabu hiyo, Todd Boehly anataka kuajiri kocha mpya baada ya kuwaalika makocha wawili wakazungumze na uongozi namna watakavyoirejeshea makali timu hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti maarufu Ujerumani la Bild, Nagelsmann alialikwa na uongozi wa Chelsea akajitambulishe na kuzungumzia mikakati yake ambayo baadaye itachujwa.

Wiki iliyopita kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Hispania, Luis Enrique alipewa ofa ya kuitembelea klabu hiyo yenye maskani yake jijini London akazungumzie kuhusu malengo na mipango yake.

Taarifa zilizoibuka Chelsea zilidai ilifikia makubaliano na Enrique, lakini mabosi wa klabu hiyo wanasubiri kuonana na Nagelsmann kwanza kabla ya kutoa uamuzi wamchuke nani. Nagelesmann anapewa nafasi kubwa ya kubeba mikoba ya Potter licha ya kufukuzwa Bayern.

Endapo kocha huyo atateuliwa ataungana na Christopher Vivell ambaye aliteuliwa na Chelsea kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Hoffenheim kabla ya kuungana tena RB Leipzig msimu wa 2019-2021.

Meridianbet yazifikia timu mbili za wanawake na kuwapa vifaa vya michezo
Dkt. Mwinyi ahimiza kuwasaidia watu wenye uhitaji