Wakala wa Mbegu za kilimo – ASA, unatarajia kuzalisha tani 4,000 za mbegu kwa msimu huu wa kilimo ikiwa ni moja ya mafanikio yaliyopatikana baada ya ongezeko la bajeti ya wakala huo ya mwaka wa fedha 2022/23 kufikia Shilingi bilioni 47.
Takwimu hizo zimetajwa hivi karibuni mkoani Morogoro na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo, Dkt. Sophia Kashenge wakati akizungumza na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kuhusu shughuli zinazofanywa na wakala huo.
Amesema kuwa, Wakala huo unafanya kazi kwa kupitia mashamba ya Serikali ambayo mpaka sasa yapo mashamba 16 na kati ya hayo, mashamba 13 yanafanya kazi na mengine matatu bado hayajakamilishwa umiliki wake huku yote yakiwa na jumla ya hekta 20,000.
“Mwaka wa fedha 2017/18 tulikuwa na bajeti ya Shilingi bilioni 1 ambapo tuliweza kuzalisha tani 500 tu za mbegu, Serikali imeendelea kutuongezea bajeti ambapo kwa mwaka 2021/22 tulipata Shilingi bilioni 10, pamoja na matumizi mengine, tuliweza kuzalisha tani za mbegu 3,200 na kwa mwaka huu tunategemea kuongeza uzalishaji kufikia tani 4,000,” amesema Dkt. Kashenge.
Aidha, ameafanua kuwa, mwaka 2017/18, ASA ilikuwa na mashamba nane ambapo kati yake, matatu tu ndiyo yalikuwa yanafanya kazi na sasa ina mashamba 16 na mashamba 13 yanafanya kazi, palikuwa na trekta moja lakini sasa kuna matrekta 14 ambapo kati yake nane ni mapya na mengine yamefufuliwa.
Hata hivyo amesema mategemeo ya ndani ya mwaka huu unaoendelea yataongezeka mara mbili yake ili angalau kila shamba liwe na trekta moja na kupitia ongezeko la bajeti, ASA imeweza kufungua mashamba pori na kuongeza mashamba mapya ili kuendelea kupunguza ongezeko la mahitaji ya mbegu nchini.