Timu ya Taifa ya Wanaume ya mpira wa Kikapu, leo Alhamis (April 20) imeanza mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya Kanda ya Tano Afrika, yanayotarajiwa kufanyika Mei 17 hadi 23, mwaka huu.

Mashindano hayo yatakayoshirikisha nchi za Somalia, Misri, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Tanzania, yatafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumzia hatua ya kuanza mazoezi ya kikosi chake Kocha Mkuu Mohammed Mbwana, amesema ameanza kukiandaa kikosi chake kuhakikisha kinafanya vyema katika mashindano hayo.

“Tumeanza mazoezi leo, wachezaji watakuwa wanakwenda na kurudi kwa wale waliopo Dar es Salaam wakati tukisubiri mwongozo wa kuweka kambi,” amesema Mbwana.

Kocha huyo amesema wachezaji waliopo mikoani na wa nje ya nchi watafanya mazoezi binafsi huku wakisubiria kukamilika kwa taratibu za kambi ya pamoja.

Timu hiyo inaundwa na wachezaji Alibani Andrew, Bernard John, Joseph Peter Mussa Chacha, Salehe Buruhani, Ally Mohamed, Baraka Sadiki, Erick Lugora, Tyrone Edward, Amin Mkosa, Denis Chibula, Enerico Augustino, Salmin Juma.

Wengine ni Fadhili Chuma, Haji Mbegu, Jackson Brown, Disco George, Atiki Ally, Fotius Ngaiza, Hashim Thabeet, Jimmy Brown na Mwalimu Heri.

Andrew Simchimba aota ufungaji bora ASFC
Tanzania kushirikiana na EAC ulinzi rasilimali za uvuvi