Bondia Twaha Kiduku amesema haikuwa rahisi kumshinda mpinzani wake kutoka Georgia Iago Kiziria katika pambano la kuwania Ubingwa wa UBO Inter-Continental lililopigwa juzi Jumamosi (April 22) mkoani Morogoro.
Kiduku ameshinda pambano hilo ambalo limepigwa katika uzani wa Super Middle huku likiwa na upinzani mkali kutokana mabondia kushambuliana kwa zamu kabla ya Kiduku kutangazwa mshindi wa pambano hilo kwa majaji wote watatu.
Katika pambano hilo ambalo lilikuwa na upinzani mkali kutoka kwa mabondia wote wawili huku Kiziria akionekana kuwa na nguvu kutokana na kupokea ngumi nyingi lakini hakuna ambayo iliweza kumpeleka chini.
Baada ya ushindi huo, Kiduku amesema: “Nawashukuru mashabiki wangu wa kujitokeza katika pambano na kuweza kunipa sapoti kubwa ambayo imenipelekea kuweza kutetea mkanda wangu wa ubingwa pamoja na kushinda ubingwa mwingine wa PST.
“Kuhusu mpinzani kiukweli hakuwa wa kawaida kwa sababu ana nguvu na alikuwa akitumia maarifa yake kuweza kunipiga lakini nashukuru Mungu nimefanikiwa kutetea pamoja na kushinda ubingwa mwingine,”
Mbali na kutwaa ubingwa wa UBO Inter-Continental, Twaha Kiduku alishinda mkanda mwengine mpya wa Ubingwa PST katika pambano hilo la raundi kumi lililopigwa kwenye Ukumbi wa Tanzanite hapa Morogoro.