Meneja wa Klabu ya Bayer 04 Liverkusen Xabi Alonso ameibukia na kupewa nafasi kubwa ya kuwa Meneja ajaye wa West Ham United, endapo David Moyes ataachana na Wagonga Nyundo wa London.

Meneja huyo wa sasa wa West Ham, ameanza michakato ya msimu ujao jambo linalofichua kwamba hana mpango wa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

Lakini, kama West Ham na Moyes wataamua kuachana, gwiji wa Liverpool, Alonso atawekwa kwenye mpango wa kuchukua timu hiyo yenye maskani yake makuu jijini London.

Xabi, ambaye ni kiungo wa zamani wa FC Bayern Munich, akiwa na umri wa miaka 41, tayari ameweka jina lake juu kwenye ukocha baada ya kuibadili Bayer Leverkusen ikiwa ni kazi yake ya kwanza kwenye Benchi la Ufundi.

Wakati Alonso alipotua klabuni hapo mwezi Oktoba mwaka jana akitokea Real Sociedad alikokuwa akiinoa timu B, Leverkusen walikuwa wanashika nafasi ya pili kutoka mkiani katika msimamo wa Ligi ya Ujerumani ‘Bundesliga’.

Lakini kwa sasa wapo kwenye timu sita za juu na imetinga Nusu Fainali ya Europa League jambo linalomfanya Alonso apite kwenye njia nzuri za kujiimarisha katika ukocha kama ilivyo kwa vijana wengine Mikel Arteta wa Arsenal na Vincent Kompany wa Burnley.

Uzoefu alionao Alonso kwenye Ligi Kuu England ni wakati alipokuwa mchezaji wa Liverpool kwa misimu mitano, ambapo aliisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA.

Alonso pia alishinda ubingwa wa Ulaya na La Liga alipokuwa na Real Madrid kabla ya kwenda kubeba Bundesliga mara tatu na FC Bayern Munich.

Thomas Tuchel ataja sababu za kichapo
Twaha Kiduku: Iago Kiziria si wa mchezo mchezo