Kiungo wa Simba SC Mzamiru Yassin amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Wydad AC umewaaminisha inawezekana na watafikia lengo lao la kutinga hatua ya Nusu Fainali wanayoisaka zaidi ya miaka minne.

Simba SC wanatarajia kurudiana na Wydad AC Jumamosi (April 29) mjini Casablanca-Morocco, wakiwa na mtaji wa ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Mzamiru amesema kitendo cha kumfunga bingwa mtetezi ligi ya Mabingwa Afrika ni rekodi kubwa kwao na imewapa nguvu ya kuamini inawezekana.

“Tumeifunga timu kubwa na mimi nikiwa miongoni mwa wachezaji waliocheza dakika zote 90 ni rekodi kubwa kwetu bado tuna dakika nyingine 90 ngumu kuhakikisha tunatinga hatua inayofuata.”

“Mengi yanazungumzwa hatuyapi nafasi tunachokiangalia sasa ni namna tutakavyojiandaa kuwakabili kwa dakika nyingine 90 ngumu kwetu tukiwa mbele kwa bao moja.” Amesema Mzamiru

Simba SC inatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam Alhamis (April 27) kuelea Morocco tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utamtoa mshindi wa jumla atakayecheza Nusu Fainali.

Simba SC itapaswa kulinda ushindi wake wa 1-0 pamoja na kusaka ushindi mwingine, huku wenyeji wao Wydad AC ikihitaji mabao 2-0 ama zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Nusu Fainali.

Mchungaji Mackenzie ni gaidi, afunguliwe mashitaka - Ruto
Thomas Tuchel ataja sababu za kichapo