Tanzania kupitia Bodi ya Filamu imesaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushrikiano na Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa (BFIC) kutoka nchini Korea Kusini kwa ajili ya uendelezaji wa tasnia ya Filamu  hapa nchini katika eneo la uandaaji na utengenezaji  wa filamu bora.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana ameshuhudia utiaji Saini wa Makubaliano hayo uliofanyika leo Aprili, 24, 2023 jijini Dodoma ambapo amesema makubaliano hayo yatasaidia kuibua fursa kwa wadau wa Filamu kupata mafunzo kuhusu namna ya kutengeneza Filamu bora zitakazopata nafasi katika soko la ndani na nje ya Tanzania.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt.Pindi Chana akishuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Taasisi ya Mashirikiano Kimataifa (BFIC) kutoka Korea Kusini leo Aprili 24, 2023 Mtumba jijini Dodoma.

Amesema, “namshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta zetu. Tanzania sasa ni ya pili katika Sekta ya filamu ikitanguliwa na Nigeria, kwa siku inazalisha Filamu nne.  Kupitia makubaliano haya, tunaamini tutaongeza Idadi na filamu zetu zitakua na ubora zaidi kuliko ilivyo sasa kutokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uandaaji ”  

Aidha, amewataka waaandaji wa Filamu nchini Tanzania watengeneze Filamu zinazozingatia maadili ya Kitanzania ambazo zinatangaza Utamaduni na lugha ya Kiswahili ili Dunia izidi kuifahamu Tanzania huku Naibu Katibu Mkuu kutoka Taasisi hiyo   Bw. Chi Lee ameeleza kuwa  Taasisi hiyo ipo tayari kuisaidia Tanzania katika Sekta ya filamu kwa kutoa Wataalam watakaosaidia kutoa mafunzo kwa waandaaji na waigizaji wa Filamu nchini Tanzania.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo ameeleza kuwa makubaliano hayo ni mafanikio yaliyotokana na ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Korea Kusini ambayo imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa ubora wa tasnia ya filamu nchini.

Rais Mwinyi aomba usafiri wa maji Pemba, Tanga
Gary Neville: Wachezaji watatu Arsenal wajitafakari