Kiungo Mshambuliaji wa Klabu ya Chelsea, Raheem Sterling atalipia gharama za masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi 14 masikini.
Winga huyo kutoka England atatoa msaada huo wa malipo ya masomo kwa vijana weusi wenye asili ya Afrika na Caribbean ambao wanatoka kwenye familia zisizojiweza.
Jambo hilo limeibuka baada ya kuwapo kwa ripoti kuna idadi ndogo isiyofikia asilimia tano ya Waingereza wanaoanza elimu ya shahada kwa wanafunzi weusi katika Vyuo Vikuu 24 bora vya Uingereza.
Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Sterling atagharimia gharama za wanafundi saba katika Chuo Kikuu cha Manchester na kile cha King’s College London.
Ofa hiyo imetolewa kwa vijana wanaoishi Greater Manchester na London.
Rais wa Chuo Kikuu cha Manchester, Prof Dame Nancy Rothwell, alisema pesa hiyo itasaidia wanafunzi weusi wenye vipaji kufikia malengo yao.
Baba huyo wa watoto wanne, Sterling, 28, alisema: “Natumaini hii kitu itabadili hali ya mambo.”
Kila kitu kitafanyika kwa kupitia Wakfu wa Raheem Sterling na mwenyekiti wake, Clive Ellington alisema: “Tunaamini jambo hilo litawafanya kupata elimu na nafasi za ajira.”