Kocha kutoka nchini Argentina Mauricio Pochettino anajiandaa kutangazwa kuwa Meneja mpya wa kikosi cha Chelsea muda wowote ndani ya wiki hii.

Meneja huyo wa zamani wa Tottenham inaaminika kwamba ataweza kuwabadili wababe hao wa Stamford Bridge kuwa washindani wa ubingwa wa Ligi Kuu England kuanzia msimu ujao 2023/24.

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 51, kwa sasa anashika nafasi ya kwanza kwenye uwezekano wa makocha wanaoweza kupewa kibarua cha kurithi mikoba ya Graham Potter huko Stamford Bridge.

Kocha wa kipindi cha mpito, Frank Lampard ataendelea kukaa kwenye benchi la timu hiyo wakati leo Jumatano (April 26) watakapokipiga na Brentford.

Lakini, mmiliki mwenza wa Chelsea, Todd Boehly amekuwa na mazungumzo ya kina na Pochettino kuhusu kumfanya kuwa kocha wake wa tano kwenye kikosi chake tangu alipoanza kuimiliki miamba hiyo majira ya kiangazi mwaka jana.

Pochettino akitua Chelsea anatarajia kuandamaa na wasaidizi wake wa siku nyingi Jesus Perez, Toni Jiminez pamoja na mwanaye mwenye sayansi ya michezo, Sebastiano.

Pochettino, Luis Enrique na Julian Nagelsmann wote hawana kazi kwa sasa na walifanyiwa usaili kwa ajili ya kibarua cha kuinoa Chelsea, lakini kocha wa zamani wa FC Bayern Munich, Nagelsmann anaripotiwa kujiweka kando kwenye orodha hiyo.

Lakini, Poch, ambaye aliinoa Spurs kwa miaka mitano yeye amekuwa hana kazi tangu majira ya kiangazi ya mwaka jana alipoachana na Paris Saint-Germain, ndiye anayepewa nafasi ya kutua London kuwa bosi wa The Blues.

Uanzishwaji programu vituo atamizi ni maono ya Rais - Silinde
Mtoto Mustapha afika Ikulu kumshukuru Rais Samia