Uongozi wa klabu ya Azam FC umepanga kuweka mikakati kabambe kuhakikisha timu yao msimu ujao inafika hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kwa mara ya tatu mfululizo Tanzania itawakilishwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa, mbili zitashiriki Ligi ya Mabingwa na mbili nyingine zitashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin maarufu kama ‘Popat’ amesema ili kufikia lengo hilo wamepanga kuboresha kikosi cha timu hiyo kwa kufanya usajili wa nguvu.
“Tumeshaanza mikakati ya kukiboresha kikosi chetu, hii inatokana na uhakika wa kushiriki michuano hiyo mwakani kwani tunashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu lakini pia tupo hatua ya Nusu Fainali kwenye michuano ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) na Tanzania itaendelea kuingiza wawakilishi wanne michuano ya kimataifa,” amesema Popat.
Amesema mbali na kutaka kukiboresha kikosi chao lakini pia wapo katika mpango kabambe kumsaka kocha mkuu atakayekiongoza kikosi chao msimu ujao baada ya sasa timu hiyo kuwa chini ya Kocha wa muda, Dani Cadena na msaidizi wake, Kally Ongala.
Amesema mchakato wa kumsaka kocha huyo unaendelea vizuri na mara baada ya msimu huu utakapomalizika watakuwa wamekamilisha.