Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ameongoza wananchi wa Mkoa wa Iringa katika kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuhimiza Watanzania kuuenzi Muungano kwa kudumisha Amani.
Akizungumza na wananchi wa mkoa huo katika Uwanja wa Samora, Dkt. Jafo amesema kuwa matunda ya Muungano yanaonekana kutokana na huo imara na wa mfano duniani ukilinganisha na nchi zingine zilizowahi kuuungana na hatimaye kutengana.
Amesema kupitia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wananchi wanaishi kwa amani na mshikamano na kutokana na hali hiyo Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Waziri Jafo amesema Watanzania wanapaswa kujivunia Muungano ambao ni tunu ya taifa letu ambapo maendeleo yanapatikan kupitia miradi ya sekta mbalimbali ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi.
“Ndugu zangu lazima tumwombee Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani tunaona miradi mingi inatekelezwa na nchi yetu inasonga mbele ambayo hakika inajenga uchumi na hayo yote ni kazi kubwa hivyo iliyofanyika chini ya uongozi wake, na tuna kila sababu ya kujivunia na kutembelea kifua mbele,”
amesisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Jafo ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kufanya vizuri katika utunzaji wa mazingira ambao ni ajenda muhimu katika mustakabali wa nchi na kutoa rai kwa wananchi hususan wa wilaya ya Mufindi kuendelea kupanda miti kwa wingi ili kunufaika na Biashara ya Kaboni ambayo tayari Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Kanuni na Mwongozo wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema katika kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu kuadhimisha sherehe za Miaka 59 ya Muungano mkoa huo umeratibu shughuli za hifadhi ya mazingira.
Amesema kuwa kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametoa jumla ya miche 89,000 lengo likiwa ni kuwakabidhi wanafunzi wa shule ili waipande na kuitunza hivyo kushiriki kikamilifu.