Mawaziri wa michezo kutoka katika nchi 14 za Kanda ya Tano ya Afrika wanatarajia kukutana jijini Arusha kuanzia Mei Mosi kujadili kwa kina namna ya kuboresha michezo katika ukanda huo.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Said Yakubu amesema kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo baada ya kutuma maombi na kukubaliwa.

Yakubu amesema kuwa Mkutano wa Baraza la Michezo la Afrika Kanda ya IV ngazi ya Mawaziri mara ya mwisho ulifanyika nchini Uganda mwaka 2018 kabla ya kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 na kuharibu mambo mengi na kwa sasa kufanyika nchini.

Amesema kuwa zaidi ya wageni 100 kutoka ukanda huo watakuwa jijini hapa kuhudhuria mkutano huo.

Amesema baraza hilo ni chombo kutoka Umoja wa Afrika (AU) kinachoshughulikia michezo na kuna kanda nyingine mbalimbali ndani ya baraza hilo zinazojumuisha nchi nyingine ambazo ni wanachama wa AU.

Amesema washiriki wa mkutano huo ni Mawaziri wa Michezo kutoka katika nchi hizo 14, ambao ni wanachama wa baraza hilo Kanda ya Tano na mkutano huo wa mawaziri utatanguliwa na ule wa wataalamu ambao ni wakurugenzi wa michezo kutoka nchi hizo.

Nchi zinazounda Kanda ya Tano ya Afrika ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea, Somalia, Djibouti Mauritius, Madagascar, Comoro na Shelisheli.

Reece James, Mason Mount ndio basi tena
Wanotesa watu wachukuliwe hatua- Majaliwa