Kocha Mkuu wa Young Africans Nasredinne Nabi, amesema licha ya kupata ushindi wa 0-2 ugenini dhidi ya Rivers United nchini Nigeria, haimaanishi kuwa wameshafuzu hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans ilichomoza na ushindi huyo Jumapili(Aprili 23) na kutanguliza mguu mmoja Nusu Fainali ya michuano hiyo.
Mwishoni mwa juma hili (Jumapili Aprili 30), Young Africans itakuwa nyumbani katika Uwanja wa Benjain Mkapa jijini Dar es salaam, kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, ili Dar kumalizia hesabu za kwenda Nusu Fainali.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema: “Tumepata ushindi mzuri tukiwa ugenini, lakini hiyo haimaanishi kuwa tumeshamaliza na tumeingia nusu fainali, vita bado ni mbichi.”
“Bado tuna mchezo mmoja mkononi, mchezo ambao naamini utakuwa mgumu zaidi ya uliopita kwa sababu Rivers hawawezi kukubali kupoteza tena kwa mara ya pili na kuondolewa kwenye michuano hii kirahisi.”
“Kwa hiyo tutakuwa na maandalizi makubwa ya kufanya ili kuhakikisha tunafanya vizuri katika uwanja wetu wa nyumbani na hatimaye kuingia nusu fainali.”