Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa Rais Kagame na ujumbe wake watawasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stergomena Tax atawapokea.
Taarifa ilieleza kuwa Rais Kagame atakwenda Ikulu kuzungumza na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan na baada ya hapo viongozi hao kwa pamoja watazungumza na waandishi wa habari kueleza waliyojadiliana na kuafikiana.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano imara wa nchi hizo mbili uliodumu kwa muda mrefu na ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo biashara za nishati, uchukuzi, elimu na utamaduni.
Hii si mara ya kwanza Rais Kagame kufanya ziara nchini kwani aliwahi kuzuru mwaka 2018 na baadaye mwaka 2019 alikuja tena nchini.
Ziara ya Rais Kagame inafuatia ziara ya Rais Samia aliyoifanya nchini Rwanda mwaka 2021.