Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka nchini Kenya, imesema Polisi wamemkamata Mchungaji maarufu wa kanisa la New Life Prayer Centre, Ezekiel Ombok Odero katika mtaa wa Mavueni mjini Kilifi, akituhumiwa kuhusika na vifo vya watu 98 vilivyotokea katika kanisa la Good News International Ministry la Mchungaji Paul Mackenzie.

Mchungaji huyo, pia anatuhumiwa kuhusika na vifo vingine vilivyotokea katika Kanisa lake kwa kushawishi waumini wake kutorosha ndugu zao ambao ni wagonjwa waliopo Hospitalini na kuwapeleka kwake kwenda kuombewa.

Mchungaji, Ezekiel Ombok Odero. Picha ya DN.

Pastor Ezekiel anatuhumiwa kuwa mshirika wa karibu wa Mchungaji Paul Mackenzie kwa kufanya mahubiri potofu ya kushawishi watu kufunga hadi kufa, huku ikidaiwa kuwa mmoja wa wachungaji wasaidizi wa Ezekiel alisema Mchungaji Mackenzie amekuwa akifadhiliwa na Pastor Ezekiel na walikua ni washirika.

Mbele ya ofisi ya DCI, Mchungaji huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, amesema Mchungaji Mackenzie alikua akilazimisha watu kufunga hadi kufa, na walipokufa Pastor Ezekiel alienda usiku wa manane kuchukua baadhi ya viungo vyao kabla ya kuzikwa.

Mchungaji, Paul Mackenzie. Picha ya NMG.

Katika kuthibitisha madai hayo, inasemekana kuwa wakati wa zoezi la ufukuaji miili, baadhi ya maiti zilikutwa bila viungo kama sehemu za siri, ulimi, figo, ini na moyo na hivyo kuleta maswali ambayo sasa yanapatiwa majibu la labda kutokana na mfanano wa matukio hayo.

Aidha, inadaiwa kuwa akaunti za benki za Mchungaji Mackenzie pia zimekutwa na kiasi cha Ksh Milioni 315, ambazo ni sawa na Tsh Bilioni 5.5 huku ofisi ya DCI ikishuku huenda zimetokana na biashara haramu ya viungo vya binadamu ambapo zoezi la ufukuaji wa makaburi limesitishwa kwa muda kutokana na kukosekana nafasi ya kuhifadhi miili.

Migogoro: Ulinzi na usalama kusimamia matumizi bora ya ardhi
Mabilioni ya JICA kusaidia ununuzi pembejeo za Kilimo, kufufua TAFICO