Akili na Maarifa ya Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ rasmi vinageukiwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, baada ya kikosi chake kutolewa katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Usiku wa kuamkia leo Jumamosi (Aprili 29), Simba SC iliondoshwa kwenye Michuano hiyo na Wydad AC kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati, baada ya matokeo ya jumla ya 1-1, mchezo ukipigwa Uwanja wa Mohamed V nchini Morocco.

Matumaini makubwa yaliyosalia kwa Simba SC ni kutwaa Ubingwa wa ASFC, ili wasimalize wakiwa mikono mitupu msimu huu, licha ya kuwa na nafasi ya pata potea katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu, ambako wako nyuma kwa alama tano dhidi ya vinara Young Africans, huku michezo minne ikisalia.

Simba SC wapo katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 63, huku Young Africans ikikaa kileleni kwa kumiliki alama 68.

Mwishoni mwa juma lijalo Simba SC itacheza mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC katika Uwanja huru (Nangwanda Sijaona) mkoani Mtwara, ikiwa ni harakati za safari ya kuisaka Fainali ya Michuano hiyo msimu huu 2022/23.

Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho hivi karibuni alizungumza na Waandishi wa Habari na kusema: “Katika msimu huu ni lazima tuchukue makombe au moja kati ya haya tunayoshindania ili kuwapa furaha mashabiki wetu.”

“Wakati nakabidhiwa jukumu la kuifundisha Simba SC, niliomba muda wa kuitengeneza, nashukuru nikaaminiwa na kupewa, tayari timu inaanza kuonekana inacheza soka safi.”

“Lakini bado ninahitaji muda zaidi ya kuendelea kutengeneza timu, nashukuru hivi sasa muunganiko umeanza kuelewana wa wachezaji wangu,”

Simba SC inatazamiwa kurejea nchini Tanzania ikiwa na nguvu zote katika Michuano ya ASFC ambako ina uhakika wa kupambania Taji, sambamba na upande wa Ligi Kuu ambapo itamlazimu mpinzani wake Young Africans kupoteza ili awe na uhakika wa kutwaa taji hilo.

The Royar Tour yaongeza idadi Watalii, mapato - Dkt. Abbas
COSTECH yaiasa jamii kusaidia, kuwekeza kwenye ubunifu