Baada ya kutimiza mpango wa kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuitoa Rivers United ya Nigeria, Uongozi wa Young Africans umesisitiza kuhamishia nguvu na maarifa kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Young Africans ilijihakikishia kucheza Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika jana Jumapili (Aprili 30), baada ya kulazimisha matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Rivers United katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliosalia kwenye michuano ya Kimataifa, wamesonga mbele katika Michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa 2-0, ambao waliuvuna wakiwa Nigeria majuma mawili yaliyopita.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amebainisha kuwa kazi bado haijaisha kwenye Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, licha ya kufikia mafanikio makubwa ya kucheza Nusu Fainali katika michuano ya Kimataifa.

Young Africans ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ wanaongoza Ligi wakiwa na alama 68 huku wakiwa na kibarua cha kucheza dhidi ya Singida Big Stars.

Kamwe amesema kuwa kila mipango ipo kwenye hesabu katika kufanikisha malengo yao na katika kipindi hiki wanaigeukiwa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ ambapo watacheza dhidi ya Singida Big Stars mfululizo.

“Kila mchezaji anatambua kuhusu malengo ambayo tupo nayo kwenye kutwaa mataji, tunahitaji kuona yale mataji ambayo tulitwaa msimu uliopita tunayabeba tena kwa wakati mwingine kwani bado kazi haijaisha tunarudi kivingine.”

“Mashabaiki wazidi kuwa pamoja nasi unaona kwenye ligi bado kuna mechi zimebaki ambazo hizi ni muhimu kwetu kupata matokeo na kwenye Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ pia tunakwenda kupambana kupata matokeo mazuri,” amesema Kamwe.

Young Africans itaanza kukipiga na Singida Big Stars katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara siku ya Alhamis (Mei 04) kisha Jumapili (Mei 07) timu hizo zitakipiga tena kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani Singida.

CEO Simba SC aahidi mkubwa 2023/24
Wanawake hawapewi fusra kuonesha uwezo - Bi. Ludanga