Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi ametamba ataingia kuwavaa wapinzani wao Marumo Gallants ya Afrika Kusini kivinge na sio kama alivyocheza mchezo wa marudiano dhidi ya Rivers United katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans itakipiga dhidi ya Marumo Gallants katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa Mei 10, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kabla ya kurudiana Mei 17 nchini Afrika Kusini.

Timu hiyo, imefanikiwa kufuzu hatua ya Nusu Fainali baada ya kuwaondoa Rivers United ya nchini Nigeria kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0 ambayo waliyapata ugenini, mabao yote yakifungwa na Mkongomani Fiston Mayele.

Kocha Nabi amewataka mashabiki waondoe hofu baada ya sare ya nyumbani dhidi ya Rivers United, kwani amepanga kuingia kwa staili ya tofauti atakavyocheza dhidi ya Marumo Gallants kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Nabi amesema kuwa alivyocheza mchezo huo wa marudiano alicheza kwa kujilinda zaidi nyumbani, akiamini wapinzani wake Rivers United wangeshambulia na kupata bao la mapema ambalo lingewavuruga, kwani hawakuwa na cha kupoteza katika pambano hilo lililomalizika kwa suluhu.

Ameongeza kuwa kwa siku chache alivyoifuatilia Marumo Gallants amegundua ni timu yenye wachezaji wazuri wanaoshambulia wakati huo wakijilinda huku wakitumia udhaifu wa mabeki katika kupata ushindi wa mapema.

“Nimeshatengeneza mpango mkakati wa kucheza dhidi Marumo Gallants tutakapocheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza hapa nyumbani kabla ya kurudiana kwao ili kuhakikisha tunafuzu kucheza Fainali.”

“Mashabiki waondoe hofu ya sisi kupoteza mchezo huu wa kwanza tutakaoanza kuucheza dhidi ya Marumo Gallants hapa nyumbani, kwani sare tuliyoipata hapa dhidi ya Rivers United ilikuwa ni ya mkakati maalum.” amesema Nabi.

Kampuni za madini zasisitizwa kutoa ajira, zabuni kwa Watanzania
Young Africans: Tunazitaka pointi tatu Singida