Kocha Mkuu wa KMC FC Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ameanza kupiga hesabu za kushinda michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia msimu huu 2022/23, huku akionyesha matumaini kwa vijana wake na morali waliyo nayo na kiu ya ushindi.

Julio aliyekabidhiwa majukumu ya kuiongoza timu hiyo hivi karibuni akichukuwa nafasi ya Kocha Hitimana Thiery, tayari ameiongoza KMC FC katika mchezo mmoja dhidi ya Dodoma Jiji na kukumbana na kipigo cha bao 1-0.

Julio amesema licha ya kuanza vibaya ni matokeo aliyotarajia kutokana na ugeni aliokuwa nao na pia hali ya wapinzani wao Dodoma Jiji, hivyo kwa sasa haoni tena wakipoteza tena mechi yoyote.

Amesema kwa sasa akili na nguvu zao zipo kwenye mechi ijayo dhidi ya Singida BS, huku akieleza kuwa maandalizi waliyonayo ikiwamo michezo ya kirafiki inaongeza morali na kujiamini kwa vijana.

“Tumekuwa na maandalizi ikiwamo michezo ya kirafiki dhidi ya Azam FC tuliyopata sare ya 1-1, hiki ni kipimo kwetu katika mwendelezo wa kujiweka fiti na mchezo ujao dhidi ya Singida Big Stars, tunahitaji ushindi katika michezo iliyobaki.”

“Mashabiki na wadau wote wa soka wa KMC FC, wawe na matumaini na timu yao, kwa muda nilionao kwa sasa naona mabadiliko mazuri ya kutia matumaini hatutaki hata play off,” amesema Julio

Hadi sasa KMC ipo nafasi ya 14 kwa kufikisha alama 28 na imebakiza michezo mitatu ikianza na Singida Big Stars, Mei 12 nyumbani kisha itasafiri kuelekea jijini Mbeya kuzifuata Tanzania Prisons na kuhitimisha na Mbeya City.

Dkt. Mkama ataka uadilifu, kupunguza matumizi ya zebaki
Sababu kupanda kwa bei za vyakula nchini yatajwa