Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, amesema wachezaji wake wanapaswa kusahau mafanikio waliyoyapata katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Rivers United, ili kuweza kufanya vizuri kwenye hatua ya Nusu Fainali ya michuano hiyo.
Young Africans imefuzu kucheza hatua hiyo baada ya kufanikiwa kuiondosha Klabu ya Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0 iliyoyapata ugenini kabla ya kutoka suluhu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam mwishoni mwa juma lililopita.
Kocha Nabi amesema wanaendelea kuwaandaa wachezaji wao kuweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Marumo Gallants FC ya Afrika Kusini na makosa yoyote watakayoyafanya ndani ya uwanja yatawagharimu.
“Tunafahamu mchezo wetu utakuwa mgumu, wachezaji lazima sasa wasahau mafanikio tuliyoyapata kwenye mchezo wa robo fainali na kujiandaa kuwakabili Marumo, hautakuwa mchezo mwepesi, kosa lolote tutakalolifanya linaweza likatuweka kwenye wakati mgumu” amesema Nabi.
Aidha, Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema hatua hiyo ya Nusu Fainali ni ngumu na kila timu iliyofuzu ni ngumu na zimejiandaa kufanya vizuri.
“Tunapaswa kumaliza mchezo hapa nyumbani, matokeo mazuri yatatupa mwanga kuelekea kwenye mchezo wa marudiano ugenini, hatua hii ni lazima tuanze kufanya vizuri kwenye mchezo wa ny- umbani,” amesema Nabi.
Young Africans itaanza mchakato wa kufuzu hatua ya Fainali kwa kuanzia nyumbani mchezo wa Nusu Fainali Mei 10, mwaka huu utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana nao wiki moja baadaye nchini Afrika Kusini.