Kikosi cha Simba SC kimeweka kambi mjini Ruangwa mkoani Lindi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC.

Simba SC itacheza mchezo huo Jumapili (Mei 07) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, huku ikidhamiria kwenda katika Hatua ya Fainali sawa na Azam FC ambayo imejiwekea malengo hayo ili kurejesha heshima ya kutwaa taji la ASFC.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema baada ya mchezo wao wa jana dhidi ya Namungo FC uliomalizika kwa sare ya 1-1, Uongozi na Benchi la Ufundi walikubaliana kikosi kuendelea kusalia mjini Ruangwa kwa ajili ya Kambi ya maandalizi ya mchezo wa Nusu Fainali ASFC.

Ahmed amesema wanaamini mazingira ya mji wa Ruangwa ni rafiki kwa kikosi chao kujiandaa na mchezo huo, huku wakiamini watakwenda Mtwara kupata matokeo mazuri ambayo yatawavusha na kuwapeleka Fainali.

“Baada ya mchezo wetu wa jana dhidi ya Namungo FC, kikosi chetu kinaendelea kusalia hapa Ruangwa kwa ajili ya kambi ya kujiwinda na mchezo wetu wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam FC, tumefanya maamuzi hayo kwa sababu mazingira ya hapa yanaruhusu.”

“Tutakuwa hapa kwa leo na kesho Ijumaa, halafu tutaanza safari ya kuelekea Mtwara kwa ajili ya mchezo wetu wa Jumapili ambao utapigwa katika Uwanja wa Nagwanda Sijaona pale Mtwara.” Amesema Ahmed Ally  

Msimu huu 2022/23 Azam FC imefanikiwa kuifunga Simba SC 1-0 katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiambulia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa Mzunguuko wa Pili.

Msimu wa 2020/21 timu hizo zilikutana katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania Bara ‘ASFC’ mkoani Ruvuma kwenye Uwanja wa CCM Majimaji, na Simba Simba SC ilipata ushindi wa 1-0, bao likifungwa na Jose Luis Miquissone.

LATRA yabariki safari za mabasi usiku, wamiliki waitwa
Kondoa watakiwa kukamilisha ujenzi Juni 2023