Kocha Mkuu wa Simba SC SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ amefunguka kuhusu makosa yaliyofanywa na Mlinda Lango Ally Salim katika mchezo na Namungo FC na kusababisha wenyeji kupata bao la kusawazisha.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi juzi Jumatano (Mei 03) Simba SC ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Mshambuliaji wa DR Congo Jean Baleke kabla ya Hassan Kabunda hajaisaiwazishia Namungo FC.

Kocha Robertinho amesema hana muda wa kuanza kumtupia lawama Mlinda Lango huyo aliyechukuwa nafasi ya Aishi Manula, bali anatakiwa kupongezwa kwa jitihada kubwa alizozionyesha hadi kufikia hapa.

“Salim ni kipa mzuri sana na kijana ambaye tunaamini ni tegemeo huko baadaye sasa kitendo cha kumtupia lawama, mimi naona hakina mashiko bali tumpe moyo wa kujituma zaidi kwani hakuna mtu aliyekuwa sahihi,” amesema.

Robertinho ameongeza makosa hayo yanaweza kumtokea mchezaji yeyote hivyo ni muda wa kuangalia mbele na siyo nyuma.

“Kwenye mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa na Wydad Casablanca hatua ya Robo Fainali, Clatous Chama na Shomari Kapombe walikosa Penati na ukiangalia ni wachezaji wakubwa sasa hakuna haja ya kurushiana lawama,” amesema.

Wakati Salim akitupiwa lawama kipa huyo amechaguliwa mchezaji bora wa Simba SC kwa mwezi Aprili akiwapiku Jean Baleke na Kibu Denis.

Tangu kuumia kwa Manula, Salim amedaka michezo mitano ambapo mitatu ni ya Ligi Kuu Bara na miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ujumbe wa DRC watembelea Bandari ya Dar es Salaam
Mhubiri Kizimbani kwa kushiriki ngono na binti wa miaka 14