Meneja wa kikosi cha Manchester United, Erik ten Hag amekiri hafahamu bajeti ya usajili itakuwaje pale Dirisha la usajili litakapofunguliwa mwishoni mwa msimu huu.

Mpaka sasa mambo bado hayaeleweki tangu klabu ilipowekwa sokoni na wamiliki wake familia ya Glazers, na inafahamika bado hawajakubali ofa iliyotolewa na Sheikh Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani na Sir Jim Ratcliffe ambao waliweka nia ya kutaka kuinunua.

Ten Hag mwenye umri wa miaka 53, amepania kuboresha kikosi chake katika Dirisha la Usajili la kiangazi na matumaini yake ni kufanya usajili wa straika mpya.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama anafahamu bajeti ya usajili ambayo ameandaliwa kwaajili ya maandalizi ya msimu ujao, Mholanzi, huyo akajibu hafahamu chochote.

“Nachofahamu kwasasa Man United ni kati ya klabu duniani, unahitaji mtaji mkubwa kuwekeza katika klabu kubwa kama hii.”

Pia kuwa aina ya wachezaji wenye uwezo wa kukupa mafanikio, wachezaji wa viwango bora wanauzwa kwa bei ghali sana, najua ninachotaka, lakini huo sio uamuzi wangu peke yangu, klabu itahusika pia katika uamuzi, kwasasa nipo bize kuimairisha timu,” alisema.

Taarifa ziliripoti Man United imempangia mikakati Mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane ili kumnasa katika dirisha la usajili la kiangazi kwani mkataba wake unaelekea ukingoni, huku Victor Osimhen anayekipiga SSC Napoli akihusishwa.

Wakati huo huo, Bilionea kutoka Qatar, Sheikh Jassim na timu yake wameweka mezani ziada ya Pauni 800 milioni ambayo itatumika kwenye kuboresha miundombinu ya Man United ikiwa ni pesa tofauti kabisa na ile ambayo wamepanga kulipa kuinunua klabu hiyo ya Old Trafford.

Ijumaa iliyopita Matajiri wanaoitaka Man United waliwasilisha ofa zao za tatu ambazo ndizo za mwisho, huku kundi linaloongozwa na tajiri wa Qatar, Sheikh Jassim liliweka Mkwanja mrefu mezani jambo litakalowafanya kuwa kwenye nafasi ya kuchuana jino kwa jino na mtu tajiri zaidi Uingereza, Sir Jim Ratcliffe na kampuni ya INEOS.

Mkakati kudhibiti maambukizi ya VVU mama, mtoto waandaliwa
Mlinda Lango Zambia azitamani Simba SC, Young Africans