Nahodha na Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Duniani ‘Timu ya Taifa ya Argentina’ Lionel Messi ameuomba radhi Uongozi wa Paris Saint-Germain, baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu.

Messi amepewa adhabu ya kukaa nje ya Uwanja kwa Majuma mawili na Uongozi wa Klabu ya Paris Saint-Germain, baada kuonekana akiwa Saudi Arabia na familia yake bila ya ruhusa.

Messi aliondoka jijini Paris hadi Saudi Arabia kutokana na ishu za kibiashara akiwa kama balozi wa nchi hiyo, lakini Uongozi wa PSG ulichukizwa na kitendo cha staa huyo kukwepa mazoezi.

Mshambuliaji huyo amesema: “Nilifikiri tungekuwa na siku ya mapumziko baada ya mchezo kama kawaida. Nilipanga safari hii na sikuweza kughairi.”

“Naomba radhi kwa wachezaji wenzangu na nasubiri kile ambacho klabu inataka kunifanyia.”

Messi, 35, alitupia picha yake kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa nchini Saudi Arabia pamoja na familia yake wakifurahia mandhari za nchi hiyo.

PSG ilipokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Lorient mwishoni mwa juma lililopita kabla ya Messi hajakwea pipa kwenda Saudi Arabia.

Kufuatia kipigo hicho miamba hiyo sasa ipo kileleni kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Marseille ambayo ina alama 70 ikiifukuzia kwa karibu katika mbio za ubingwa.

Kitumbo, Ulimboka kikaangoni TFF
Sven Vandenbroeck kocha mpya Wydad AC