Kiungo Mshambuliaji kutoka Brazil na Klabu ya Singida Big Stars, Bruno Gomes ameamua kukata mzizi wa fitina kwa mashabiki wa klabu hiyo, kufuatia kuhusishwa na tetesi za kujiunga na Young Africans msimu ujao 2023/24.
Bruno kwenye mechi dhidi ya Young Africans ambayo Singida Big Stars ilifungwa mabao 2-0 (Alhamisi) alisalimia na na benchi zima la ufundi la Young Africans kabla mchezo haujaanza na mchezo ulipomalizika alionekana kuzungumza jambo na Kocha wa makipa wa Young Africans, Milton Nienov na kiungo timu hiyo, Stephen Aziz Ki.
Kiungo huyu pia baada ya kutoka uwanjani aliweka picha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiandika: “Daima kusonga mbele Mungu ni mwema.”
Kauli hiyo ni kama vile ilichochea uvumi wa yeye kusajiliwa Young Africans ambapo amesisistiza: “Hapana yale ni maneno ya kawaida kama ambayo huwa naandika siku zote.
“Rafiki yangu hili ni jambo la kawaida kusalimia watu kwani hata mechi zingine huwa nafanya hivyo.
Kweli nilikuwa nazungumza nao (Young Africans) baada ya mehezo lakini tulikuwa tunazungumza kuhusu mchezo wote kiujumla na siyo ishu ya usajili.”
Bruno wakati anajiunga na Singida Big Stars alisaini mkataba wa miaka miwili lakini baada ya kuonyesha kiwango bora aliongezewa mkataba mwvingine wa miaka mitatu itakayomfanya aendelee kusalia katika timu hiyo kwa muda mrefu ujao.
Kiungo huyo mwenye mabao tisa kwenye Ligi Kuu Bara anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri kwenye ligi msimu huu, kipaji chake kikizikosha timu.