Kocha Mkuu wa KMC, Jamhuri Kihwelo Julio’ amesema maandalizi yao ya kuikabili Singida Big Stars yanakwenda vizuri na ana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.

Kocha huyo ameeleza kuwa kushinda mchezo huo kutawapunguzia Presha waliyokuwa nayo hivi sasa ya kushuka daraja msimu huu 2022/23.

“Singida ni timu nzuri na ina wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, lakini huu ni mchezo muhimu kwetu hasa ukizingatia nafasi tuliyopo kwenye msimamo siyo nzuri,” alisema Julio.

Kocha huyo ambaye ameichukua timu hiyo siku chache zilizopita akirithi mikoba ya Thiery Hitimana aliyefutwa kazi kutokana na matokeo mabaya, amesema amekuwa akizungumza na wachezaji wake kuwaeleza umuhimu wa ushindi katika mechi zao tatu zilizosalia.

“Wachezaji wangu wamenihakikishia kupambana na kuondoka na pointi tatu kwenye michezo yao mitatu iliyobaki na kwa kuanzia wataanza na mechi yetu dhidi ya Singida Big Stars. Tutakuwa, nyumbani Uwanja wa Uhuru na hii ni faida kwetu,” amesema beki huyo wa zamani wa Simba SC

Julio amesema anashukuru uongozi wao upo bega kwa bega nao katika kipindi hiki kigumu wanachopitia na wao watapambana ili kuhakikisha timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni inabaki kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao.

KMC inashika nafasi ya 14 mweye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikikusanya alama 26 katika michezo 27 waliyocheza mpaka sasa kwenye ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 16.

Pialali kukiwasha Dar es salaam Mei 27
Kilimo waomba kuidhinishiwa zaidi ya Bilioni 970