Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kuna maombolezo ya kitaifa hivi leo, kuwakumbuka watu zaidi ya 400 waliopoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko makubwa, katika Wilaya ya Kalehe, mkoani Kivu Kusini, Mashariki mwa nchi hiyo, kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha.
Maombolezo haya yanafanyika wakati huu Serikali ikiendelea kukadiria hasara iliyotokana na mafuriko hayo, huku shughuli za mazishi pia zikiendelea katika moja ya majanga mabaya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo.
Aidha wengine mbali na kupoteza ndugu zao, wamesema shughuli za maisha ya kawaida zimekoma rasmi baada ya kupoteza mali nyingi ambazo walikuwa wakizitegemea kukimu familia zao huku Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu nchini DRC, wakipata miili hiyo wengi wakiwa wanawake na watoto katika kijiji cha Bushushu, mashariki mwa nchi hiyo.
Hata hivyo, bado kuna wasiwasi kuwa huenda idadi ya watu waliopteza maisha ikaongezeka kwa sababu watu wengi hawajapatikana. Théo Ngwabidje Kasi ni Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini ambapo mafuriko hayo pia yamesababisha maafa ya mamia ya watu katika nchini jirani ya Rwanda, huku mataifa mengine ya Afrika Mashariki, yakishuhudia mvua kubwa inayosababisha mafuruko na maporomoko ya udongo.
Ni siku tatu sasa tangu mafuriko yalipotokea na idadi ya waliofariki inaendelea kuongezeka ambapo sasa imefikia watu 400 huku hofu ya kuongezeka ikiwepo na wiki iliyopita nchi jirani ya Rwanda pia ilikumbwa na mafuriko baada ya Ziwa Kivu kuvunja kingo zake na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 130.