Serikali imewataka wananchi waache kujenga katika mabonde, kwakuwa maeneo hayo ni rahisi kutuama maji hivyo kusababisha mafuriko ambayo huathiri Maisha yao.

Wito huo umetolewa Bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwera, Zahor Mohamed Haji ambaye alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kudhibiti mafuriko ambayo husababisha uchafuzi wa mazingira na kuongeza umaskini katika Jimbo la Mwera.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema inahitajika pia elimu itolewe kupitia halmashauri zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar kuhusu umuhimu wa kujenga nyumba maeneo yaliyopimwa kwani kwani tayari yamekidhi vigezo vya kutumika kwa makazi.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kufanya tathmini ya kina katika maeneo yote yanayokumbwa na mafuriko nchini katika mwaka wa fedha 2023/2024.

“Tayari Serikali imechukua hatua za kuunda Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ yenye jukumu kuu la kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Wilaya wa Kukabiliana na Maafa ya mwaka 2022,” alisema.

Naibu Waziri Khamis aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na hatua za kuunda kamati hiyo pia Serikali imeendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na maafa yakiwemo mafuriko.

Lampard awakingia kifua Sterling, Hakim Ziyech
Hizi hapa sababu za Mandonga kupelekwa Dodoma