Kocha wa Ihefu FC, Zuberi Katwila, ameahidi kukiongoza kikosi chake kushinda michezo mitatu iliyobaki ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kumaliza katika nafasi salama katika msimamo wa Ligi hiyo.

Hadi sasa Ihefu FC ipo nafasi ya nane ikiwa na alama 33 baada ya kushinda michezo 10, imetoka sare katika michezo mitatu na kupoteza michezo 14.

Katwila amesema pamoja na timu yake kuwa katika nafasi nzuri, haipaswi kubweteka na kutozingatia michezo iliyobaki kwani alama tisa zilizobaki ni muhimu.

Katwila amesema mechi za mwisho zilizobaki huwa ushindani mkubwa na kama kikosi chake kitateleza kinaweza kuporomoka na kumaliza ligi kikiwa katika nafasi za mwisho.

“Ligi bado haijaisha, lazima tufanye vizuri katika mechi zote zilizobaki na kama tutazidi kutoa ushindani tunaweza kupanda au kubaki katika nafasi ya sasa,” amesema.

Ihefu inatarajiwa kushuka dimbani Mei 14 mwaka huu kumenyana na Coastal Union kabla ya kuumana na Geita Gold na itamaliza ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Nathan Ake hatarini kukosa mchezo wa kisasi
Wawili wanyongwa kwa matusi, kuchoma Kurani