Licha ya kikosi chake kuzidiwa alama moja na Manchester City ambayo ina mchezo mmoja mkononi, Meneja wa Kikosi cha Arsenal Mikel Arteta, amewataka wachezaji wake kuendelea kuupambania ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu 2022/23.

Arteta alitoa kauli hiyo baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle United katika Uwanja wa St. James Park, juzi Jumapili (Mei 07).

Mabao la Kiungo na Nahodha Martin Odegaard na Fabian Schar ambaye alijifunga, yalirejesha matumaini ya Arsenal kuendelea kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Baada ya ushindi huo, Arsenal imeshika nafasi ya pili ikiwa na alama 81 katika mechi 35 wakati Man City inaongoza ligi hiyo ikiwa na alama 82 baada ya kushuka dimbani mara 34.

Arteta ambaye ni raia wa Hispania, amesema bado kikosi chake kina nafasi ya kutwaa ubingwa huo msimu huu.

Meneja huyo amesema wachezaji wake wanapaswa kuendelea kupambana kwani anaamini mambo mazuri hayako mbali.

“Kitu pekee tunachoweza kufanya ni kuendelea kusisitiza na tusigeuke nyuma na kupoteza muelekeo wetu juu ya kitu kingine. Tuendelee kwenda na tuone nini kitatokea,” amesema

Meneja huyo alisema kikosi chake kinapaswa kuendelea kushinda katika mechi zilizobaki msimu huu.

Katika ligi hiyo, Arsenal imebakisha mechi dhidi ya Brighton, Nottingham Forest pamoja na Wolves.

Wiki ya Madini FEMATA: Majaliwa awasili Mwanza
Panga kufyeka Saba Simba SC, watatu waingia kwenye rada