Rais wa Klabu Bingwa nchini Italia SSC Napoli, Aurelio De Laurentiis, amebadili mawazo kuwa majira ya joto hawatamuuza tena Mshambuliaji wao hatari kutoka Nigeria Victor James Osimhen.
Osimhen msimu huu wa 2022-23 amekuwa lulu Barani Ulaya kufuatia uwezo wake wa kupachika mabao akifunga mabao 23 ndani ya Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, pia amekuwa chachu ya mafanikio ya SSC Napoli ambayo juma lililopita ilijihakikishia kutwaa taji la ubingwa wa ‘Serie A’ kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33 kupita.
Nyota huyo amekuwa akiwaniwa vikali na Klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England ‘Premier League’, Ligi ya Ujerumani ‘Bundesliga’ na Ligi ya Ufaransa ‘Ligue 1’.
Awali SSC Napoli ilitaja bei ya kumuuza Osimhen kuwa ni Pauni Milioni 150, lakini sasa imebadili mawazo juu ya staa huyo.
Rais wa klabu hiyo amesema: “Sitamuuza Victor Osimhen kipindi cha majira ya joto, hilo halitabadilika, itabaki hivyo na atakuwa hapa kwa msimu ujao.”
Osimhen msimu uliopita kwa mara ya kwanza aliibuka kuwa mchezaji bora mdogo ndani ya Serie A, lakini msimu huu huenda akamaliza ligi akiwa mfungaji bora wa ligi hiyo.