Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa kiungo wao, Mzambia Clatous Chama hajaandika barua yoyote ya kuomba kuondoka na badala yake ataendelea kuwepo klabuni hapo katika msimu ujao.

Jana Alhamis (Mei 11) taarifa zilizagaa za kiungo huyo kuwaandikia barua ya kuwaaga viongozi wa timu hiyo, kuwa hatakuwa sehemu ya wachezaji watakaoichezea Simba SC katika msimu ujao.

Simba SC imepanga kukiboresha kikosi chao kwa kufanya usajili mkubwa na kisasa watakaowawezesha kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu ujao.

Ahmed amesema kuwa hizo zinazoendelea ni tetesi pekee ambazo mashabiki wa Simba SC wanatakiwa kuachana nazo na badala yake kuelekeza nguvu katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara waliyoibakisha.

Ahmed amesema kuwa uongozi haujapokea barua yoyote kwa Chama ya kuomba kuondoka, hivi sasa kambini akiendelea na maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting watakaoucheza leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.

Ameongeza kuwa hivi sasa wanajipanga upya kuhakikisha wanarudi katika utawala wao kwa kufanya usajili bora utakaowafikisha Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hizo taarifa za Chama kuandika barua kwa uongozi nazisikia kuomba kuondoka mara baada ya ligi kumalizika, lakini kwa uongozi bado hazijafika.

“Niwaondoe hofu mashabiki wa Simba kuwa Chama ni mchezaji wetu na ataendelea kuwepo hapo, kwani ana mkataba wa bado wa mwaka mmoja ndani ya timu. “Wanasimba tukutane Azam Complex baadae leo Ijumaa saa 1:00 usiku tumalizie kwa pamoja msimu wa 2022-2023, wakati tukijipanga upya turudi kwenye utawala wetu, tunao wajibu wa kukamilisha ratiba yetu, mkubwa hasahau njia bali anabadili uelekeo,” amesema Ahmed

Madaktari wachunguza ugonjwa usiojulikana uliouwa nane
Bares awapongeza wachezaji Tanzania Prisons