Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la soka nchini Uruguay amefichua mpango wa Shirikisho hilo kufikia makubaliano na Marcelo Bielsa, ili kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya nchi hiyo.
Jorge Casales, mjumbe wa kamati ya utendaji wa Shirikisho la Soka la Uruguay amesema Bielsa aliyekuwa meneja wa Leeds United ya England, atasaini mkataba wa kuifundisha Uruguay mpaka fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
“Kitu pekee kinachokosekana ni saini yake,” amesema Casales kuhusu mkataba wa miezi 39 aliosaini Kocha huyo mkongwe Bielsa
Mechi ya kwanza ya Bielsa akiwa kocha wa Uruguay inatarajiwa kuwa Juni wakati timu hiyo ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Nicaragua na Cuba, mechi za kufuzu Kombe la Dunia Septemba mwaka huu.
“Tunamleta ambaye tunajua atatuachia kumbukumbu itakayokwenda nje ya dakika 90,” amesema Casales
Uruguay iliondoshwa kwenye hatua ya makundi ya Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar mwaka jana.
Bielsa aliifundisha Argentina kuanzia mwaka 1998 mpaka mwaka 2004 na kushuhudia timu hiyo ikiondoshwa hatua ya makundi kwenye Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Korea Kusini na Japan mwaka 2002 na kisha akaiongoza Argentina kushinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Athens, Ugiriki mwaka 2004.
Alijiweka kando kuinoa timu hiyo kwa sababu binafsi na kuifundisha Chile kati ya mwaka 2007 na 2011.
Kocha huyo pia amewahi kuinoa Espanyol, Athletic Club na Lille. Amekuwa nje ya kazi tangu Februari mwaka 2022 alipotimuliwa na Leeds.
Casales amesema majadiliano na Bielsa yalichukua kipindi cha miezi miwili.