Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Salim Abdallah Try Again’, amekiri msimu huu 2022/23, kikosi cha klabu hiyo kumeshindwa kufanya vizuri, hivyo wanajipanga upya kuja kivingine kuelekea msimu mpya 2023/24.

Bosi huyo amesema msimu huu kulikuwa na makosa makubwa ambayo walifanya na kupelekea anguko la timu yaop ambayo lilianza miaka miwili nyuma.

“Wengi wanaangalia anguko letu kwa sasa, lakini anguko letu lilianza miaka miwili nyuma baada ya kuwaruhusu kuondoka Chama (Clatous) na Luis Miquissone hakukuwa na mbadala wao, ukiangalia tumemleta Banda (Peter) ila hakuweza kuziba nafasi yake, tunajipanga kuangalia ni namna gani tutafanya maboresho kwenye kila idara ya timu ili kuwa bora,” amesema kiongozi huyo.

Pia amewaomba radhi mashabiki na wanachama wao kwa kukosa mataji katika msimu mwingine huku akitaja majeraha yaliyowapata wachezaji wao muhimu yalichangia kuwaangusha.

“Hakuna wa kumbebesha lawama au kuwaonyesha vidole watu au viongozi waliopewa jukumu la usajili, alitolea mfano Sawadogo (Ismael) alikuwa vizuri katika Ligi ya Morocco, na alikuja Simba alionyesha kiwango kizuri lakini baadaye alipata majeraha na kushindwa kuonyesha ubora wake,” bosi huyo amesema

Ameongeza watafanya usajili mkubwa ambao unaendana na washindani wao huku akiongeza uzoefu wa viongozi na wachezaji utasaidia kutoa ushindani mkubwa katika michuano iliyopo mbele ya Super Cup.

Ameweka wazi Simba SC imeachana na kocha wa viungo, Kelvin Mandla ambaye ni raia wa Afrika Kusini huku kukiwa na tetesi za kurejeshwa kwa Adel Zrane aliyewahi kufanya kazi hiyo kwa mafanikio.

Usaidizi wa kujiuwa: Bunge lapitisha matumizi ya euthanasia
Aron Ramsdale kumwaga wino Arsenal