Meneja kutoka Argentina Mauricio Pochettino hatimaye amekubali masharti ya kuwa Mkuu wa Benchi ya Ufundi la Chelsea, na ataanza kuifundisha timu hiyo wakati wa maandalizi ya msimu mpya baada ya timu hiyo kuwa na kipindi kibaya katika Ligi Kuu kwa miaka 20 sasa.
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimebainisha kuwa makubaliano hayo yamefikiwa saa chache baada ya kikosi cha kocha wa muda, Frank Lampard kushindwa kuibuka na ushindi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge dhidi ya Nottingham Forest.
Msimu huu umekuwa mbaya zaidi kwa timu hiyo katika kipindi hicho cha miongo miwili. Chelsea imetoka sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi Forest katika ya mchezo wa Ligi Kuu juzi.
Meneja huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur hakuwemo uwanjani wakati timu hiyo ikicheza mchezo huo.
Familia yake imeendelea kubaki jijini London tangu alipoondoka Spurs Novemba mwaka 2019 alipoenda Paris.
Muargentina huyo amechukua muda wake kufanya makubaliano na wamiliki wa Chelsea, wakiongozwa na wawekezaji Todd Boehly na Behdad Eghbali.
Klabu hiyo imetumia takribani kiasi cha Pauni milioni 600 kwa ajili ya kusajili wachezaji tangu klabu hiyo ichukuliwe miezi 12 iliyopita wakati alipotimuliwa Thomas Tuchel na Graham Potter.
Inatarajiwa kuwa klabu itawekeza kwa kumsajili mshambuliaji mpya wa kati na kipa mpya.
Edouard Mendy atakayerudi tena katika kikosi hicho kuchukua nafasi ya Kepa Arrizabalaga, kukabiliana na Fores, ikiwa ni moja ya mabadiliko.
Imani ya Pochettino iko kwa Jesus Perez, Miguel D’Agostino, Toni Jimenez na mtoto wake Sebastiano ambao wote wanatarajia kutua Chelsea baada ya kocha huyo kutua Chelsea.
Chelsea imebakiza mechi tatu tu msimu huu, ambapo itakuwa ugenini dhidi ya Manchester City na Manchester United na baadae itarudi kwenye uwanja wake wa Stamford Bridge kwa ajili ya mchezo wa mwisho dhidi ya Newcastle United.
Hatahivyo, Pochettino hatarajiwi kuhudhuria mchezo wowote kati ya hiyo na Lampard ataendelea kukiongoza kikosi hicho hadi mwisho wa msimu.
Pochettino hakuwahi kupata ofa ya kurejea tena Spurs. Klabu yake hiyo inaangalia kuajiri kocha mpya.
Lampard alisema baada ya mchezo wa juzi kuwa timu yake ilikosa mshambuliaji muuaji na kushindwa kufanya vizuri katika kipindi cha kwanza. “Kitu kinachonikatisha tamaa sana ni kufanya vibaya katika dakika 45 za kwanza.
“Kilichonisikitisha zaidi ni kupoteza dakika 45 za kwanza za mchezo ambao tuliutawala zaidi, lakini tulishindwa kufanya cha maana.
“Kwa kweli sio vizuri kucheza asilimi 60 au 70 katika robo tatu ya mwisho. Robo ya mwisho unatakiwa kucheza kwa asilimia 100…”
Alipoulizwa anatarajia nini katika wiki mbili zijazo, Lampard alisema: “Nataka kuona mchezo mzuri, baadhi ya matokeo mazuri. Kitu ambacho unataka kukiona wakati wote…”