Hatimaye Meneja wa Arsenal Mikel Arteta amekubali yaishe, baada ya kuwaomba radhi Mashabiki wa klabu hiyo, kufuatia mpango wake wa kusaka ubingwa kushindikana msimu huu 2022/23.
Arsenal juzi jumapili (Mei 14) ilimaliza mwendo wa kuufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya England, kufuatia kipigo cha 3-0 kilichotolewa na Brighton katika Uwanja wa Emirates jijini London.
Kichapo hicho kilimaanisha kwamba Manchester City itatawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu kama Gunners itafungwa kwenye mchezo wao Jumamosi (Mei 20) dhidi ya Nottingham.
Arteta aliyekuwa na hasira alisema: “Nachukia kitendo cha kuwaangusha watu, wakati wakiwa na matarajio ya kupata kitu. Hilo ndilo linalonipa majuto zaidi na nalazimika kuwaomba radhi mashabiki.
“Nafasi ya pili imepatikana, na hilo haliwezi kubadilika, lakini matokeo haya yanakwenda kunipa muda zaidi wa kufikiri.
“Kazi yangu ni kupata mafanikio kutoka kwa kila mchezaji na bila shaka juzi sikufanya hivyo, hivyo hapa nawajibika.”